JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA
2011/2012
UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Pamoja na hotuba hii, vipo vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara na Idara zinazojitegemea ambapo cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2011 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Aidha, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara kubwa na nyeti, ninamuahidi kuwa sitamuangusha. Pia ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Billal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile,
ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na hatimaye kupitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi Mhe. Spika Anne Makinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Spika na hivyo kuwa mwanamke wa kwanzakuongoza Bunge katika Afrika Mashariki. Kuchaguliwa kwako kunatokana na imani kubwa waliyonayo Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia busara zako, uwezo na uzoefu wako ndani ya Bunge hili. Napenda pia kumpongeza Mhe. Job Ndugai (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Nawapongeza pia mawaziri wenzangu wote pamoja na Naibu mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda niwapongeze wabunge wote kwa kuchaguliwa na kuteuliwa kuingia katika Bunge hili.
4. Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii. Maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanahusisha wadau na vyombo mbalimbali. Kipekee ninaishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii.
5. Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru kwa namna ya pekee Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2011 na nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii. Kwa upande wa Wizara ya Fedha, nawashukuru Naibu Mawaziri, Mhe. Gregory Teu (Mb) na Mhe. Pereira Ame Silima (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu, Ndugu Laston T. Msongole, Dkt. Servacius B. Likwelile na Ndugu Elizabeth Nyambibo. Napenda kuwashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa. Aidha, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha. Vile vile, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Mwisho, nawashukuru wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
6. Mheshimiwa Spika, huu ni mkutano wa kwanza wa Bajeti kwa Bunge hili baada ya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika mwezi Oktoba mwaka 2010 na kukirejesha Chama Cha Mapinduzi pamoja na Serikali yake katika kipindi cha pili cha Awamu ya Nne. Wananchi wana matumaini makubwa kwa Bunge hili kwamba litasaidia kuongeza kasi ya kuwapatia maendeleo na kuondokana na umasikini wa kipato unaowakabili wananchi walio wengi. Hili linajidhihirisha kwa uwepo wa Waheshimiwa Wabunge wenye umri, jinsia, elimu, na uzoefu mbalimbali. Ni matumaini ya Serikali kuwa uwepo huo wa Waheshimiwa Wabunge utakuwa ni chachu katika kuwaletea maendeleo wananchi kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi.
7. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka wa fedha unaoishia 2010/2011, imeendelea kutumika kama chombo muhimu katika kutekeleza Sera na Malengo ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii. Katika kipindi hiki, yamekuwepo mafanikio ya kuridhisha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini.
8. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2011/12 itazingatia vipaumbele vifuatavyo:
i) Umeme;
ii) Maji;
iii) Miundombinu ya usafiri na usafirishaji (reli, bandari, barabara, viwanja vya ndege, Mkongo wa Taifa);
iv) Kilimo na umwagiliaji; na
v) Kupanua ajira kwa sekta binafsi na ya umma.
Bajeti itahakikisha pia kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu na afya yanalindwa pamoja na kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa.
No comments:
Post a Comment