Friday, August 24, 2012

Mume mwema na bora: Sifa na wajibu wake...

Sifa za Mume mwema:

Wapendwa wana JF wenzangu leo nimeona tuongelee sifa za mume mwema; nitasimulia/fafanua kama inavyoongelewa ki Biblia. Nimeona niweke hizi sifa hapa sio tu kwa wanandoa kukumbushana bali hata kwa vijana watarajiwa kuelewa sifa na wajibu wa mume mwema.

Nimeanza na sifa na mistari michache inayoongelea mume katika ndoa ya Kikristo.

1. Aliyesimama katika imani na tayari kuitetea katika familia:

1 Wakorintho 11:3Lakini napenda muelewe kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, kama vile mume alivyo kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo.

Waefeso 5:23Kwa maana mume ni kichwa cha mke kama vile Kristo alivyo kichwa cha kanisa, ambalo ni mwili wake, naye mwe nyewe ni Mwokozi wa kanisa.

Ikumbukwe huyu ndiye anauamuzi wa mwisho katika familia akiamua kuukana ukristo, kurudi nyuma inakuwa na athari kubwa sana katika familia. Hivyo hii ndio nguzo ya ndoa ya Kikristo.


2. Ampende mkewe:

Waefeso 5:33Hata hivyo kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake. Upendo ni nguzo ya Pili na pia ni moja ya tunda la Roho katika ndoa.

Hapa naomba nieleze hii ndoa inayoongelewa ni ya Kikristo hivyo upendo huu hauwezi kuutenga na upendo wa Kristo kwa ujumla, je upendo unaelezwaje katika Biblia:


a. Huleteana heshima Warumi 12:10
Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa kindugu. Waheshimuni wengine kuliko mnavyojiheshimu wenyewe.

b. Hufadhiliana: Atakupa mahitaji yako bila kujali nani anazalisha zaidi, hatajali cheo aua elimu yako. Maana katika ndoa mwingine anaweza panda zaidi ya mwingine lakini sio sababu ya kumwacha kwa kujiona utaonekana duni. (kuwa na kiburi)
1 Wakorintho 13:4 4Upendo huvumilia, upendo hufadhili; upendo hauna wivu au majivuno.

c. Hauna ubinafsi na kusameheana: Hatatunza maƱosa yake moyoni atasamehe na kusahau, haujihesabii haki
1 Wakorintho 13:4-8 5Upendo hauna kiburi na haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti kujipendeza nafsi; haukasiriki upesi, hauweki orodha ya mabaya.

d. Huonyana: atakwambia kama unakosea na siyo kukuacha upotee na marafiki wabaya
1 Wakorintho 13:4-8 6Upendo haufurahii mabaya, bali hufurahia kweli,

e. Hustahimiliana: hata uwe mgumba, mlemavu, unakasoro gani atakuvumilia.
1 Wakorintho 13:4-8 7Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote,

f. Hauna ukomo au mipaka: Atakupenda hadikifo sio siku anaamka ‘mimi na wewe basi” 1 Wakorintho 13:4-8 8Upendo hauna mwisho. Lakini penye unabii, utakoma; zikiwepo lugha zitakoma; yakiwepo maarifa yatakwisha.

3. Heshima na huruma:
Heshima humfanya mtu ajione unamjali, wanaume wengine atasema anapenda lakini anamwita mwenzie hajasoma, ametoka familia duni, hafanani na hali yangu, kwakweli huku ni kumdhalilisha mwenzioa
1 Petro 3: 7 – 9 7Kadhalika ninyi waume, ishini na wake zenu kwa kuwahurumia, mkitambua ya kuwa wao ni dhaifu na hivyo muwape heshima, kwa maana ninyi ni warithi pamoja nao wa neema ya uzima. Fanyeni hivyo ili sala zenu zisizuiliwe.

4. Amtimizie haja zake za kimwili:
Mume anatakiwa kujali mahitaji ya kimwili ya mke, kama mume amesimama katika imani yake ataenenda kwa roho na mke vivyo ni roho atakaewaongoza hata katika hili na si mikanda ya video, magazeti au daktari labda uwe na ugonjwa.
1 Korintho 7: 3-5: 3Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe; na hali kadhalika mke kwa mumewe. 4Kwa maana mke hatawali mwili wake mwenyewe, bali mume wake ndiye autawalaye. Vivyo hivyo, mume hata wali mwili wake mwenyewe, bali mkewe ndiye anayeutawala. 5Msinyimane, isipokuwa kama mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda mfupi ili muwe na nafasi nzuri ya maombi. Lakini baada ya muda huo rudianeni tena shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kushindwa kujizuia.

5. Ajue kulea watoto:
Mume ndiye baba pia hivyo asiishie kupenda mke tu watoto hajui wanasoma vipi, wanaishi vipi, anaacha malezi na makuzi yote kwa mama, siku watoto wakiharibika anaanza kumlaumu mama. Watoto wanahitaji wazazi wote wawili ili kukua katika mwenendo mzuri wa maadili ya Kikristo.
1 Timotheo3: 4 4Aweze kuisimamia nyumba yake vizuri akiwafanya watoto wake kuwa wanyenyekevu na wenye heshima katika hali zote. (Hata kama imetajwa kuwa ni sifa ya Askof ila imebainishwa ni moja ya sifa za mume)

6. Aiheshimu ndoa / asiwe mzinzi:
Kuna wanaume ambao anaweza kukupatia mahitaji yote muhimu, lakini ni mzinzi tena wala hafichi, hii kwakweli ndio sababu kubwa ya kuvunjika ndoa nyingi sasa hivi. Ulipoapa mbele za Mungu utampenda mwenzio hadi kifo iweje uchangie upendo huu na wengine, hapa ni kama umesema “nilikupenda lakini sasa nimepata mwingine hivyo unamruhusu aondoke katika ndoa yenu” wengine hawaishii hapa anafukuza na kuoa mwingine kabisa. Mwanamke anahitaji kuona kuwa yeye ndiye pekee anayepewa upendo huu na mumewe na sio kuchangia na msururu wa wenza.
Waebrania 13:4 Ndoa iheshimiwe na watu wote, na wenye ndoa wawe waaminifu kwa wenzi wao ; maana Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati.
Mathayo 19:9-11 9 Nami nawaambieni, mtu ye yote anayemwacha mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akaoa mke mwingine, anazini.'' [``Na mtu anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka pia anazini.'']


7. Anayejitegemea kwa kimawazo na mali:

Kuna waume ambao pamoja na umri wa kuoa bado anategemea baba, mama, kaka, dada kwa mahitaji yake na pia hata mawazo afanye nini. Sio vibaya kukaa na ndugu hasa kama ni wema na wanatabia nzuri pia wasioingilia ndoa yako. Na ni vizuri pia kupata ushauri wa waliotuzidi katika mambo mbalimbali unayotaka kufanya lakini isiwe ni kikwazo cha upendo, heshima na uhuru wa ndoa yenu. Mume awe anajitegemea awe mbunifu akimshirikisha mkewe ili pamoja waweze kujitegemea na sio kutegemea wazazi hadi kutawaliwa hapa hata uimara wa Imani yake unaegemea huko anakofadhiliwa.

Marko 10:7Na kwa sababu hii mume atamwacha baba yake na mama yake na hao wawili, watakuwa mwili mmoja.

Hapa ina maana aweze kumtunza mkewe na familia pamoja na kumwezesha.

Mbarikiwe

No comments:

Post a Comment