Friday, August 17, 2012

UTUKUFU WA BUNGE LA TANZANIA

Kama tunavyofahamu bunge letu linajulikana kama ni bunge tukufu la Tanzania. Kwa maoni yangu ukipitia maamuzi mengi ndani ya bunge hili sioni utukufu wowote wa kustahili kuliita bunge letu ni Bunge tukufu la Tanzania. Kipi walichokifanya tangu wateuliwe katika uchaguzi wa 2005 ambacho kinaonyesha utukufu wa Bunge hilo? Ukiondoa wabunge wachache wa CCM ambao hawafiki hata 10 na wabunge wote wa upinzani naweza kabisa kutamka kwamba Bunge hilo halina utukufu wowote. Nasema kwamba Bunge letu halina utukufu wowote kwa sababu mbali mbali na nitazitaja hapa. Bunge hilo limeendelea kuwakumbatia mapapa mafisadi ndani ya Bunge hilo akiwemo Lowassa aliyehusika moja kwa moja na tuhuma za ufisadi wa Richmond/Dowans. Karamagi ambaye pamoja na bunge hili kufikia makubaliano kwamba mkataba wa kampuni yake ya TICTS na serikali uvunjwe tangu mwaka 2008 hadi hii leo hakuna ufuatiliaji wowote ndani ya Bunge ili kujua kwanini serikali hadi hii leo haijavunja mkataba huo pamoja na kushauriwa kufanya hivyo na Bunge. Na pia alihusika katika kuudanganya umma wa Tanzania kuhusu mkataba wa uchimbaji dhahabu wa Buzwagi. Rostam Azizi ambaye ana tuhuma mbali mbali za ufisadi wa mabilioni kupitia Richmond/Dowans, Kagoda na pia inasemekama yumo pia kwenye Meremeta na Tangold. Chenge au kwa jina maarufu la "Mzee wa Vijisenti" ambaye pamoja na kugundulika kwamba alijipatia fedha haramu katika ununuzi haramu wa rada ambao ulipigiwa debe sana na mafisadi Mkapa na Mramba. Kama mtakumbuka kauli ya fisadi Mramba kwamba "Hata majani tutakula lakini Rada lazima inunuliwe" sina haja ya kuandika zaidi yaliyojiri katika ununuzi huo haramu wa rada. Fisadi Mkono ambaye alilipwa bilioni 8 na BoT ambazo hadi hii leo ameshindwa kuthibitisha alifanya kazi gani BoT kwa muda gani hadi kustahili kulipwa pesa nyingi kiasi hicho. Pamoja na Gavana kuunda tume ya kufuatilia uhalali wa Mkono kulipwa mapesa hayo yote, hadi hii leo Gavana Ndullu hajatwambia kuhusu hatma ya kazi aliyowapa kamati hiyo. Fisadi Mzindakaya ambaye alipatiwa mkopo wa mabilioni na BoT pamoja na kuwa bank hiyo haihusiki kutoa mikopo kwa watu binafsi kwani kazi hiyo hutakiwa kufanywa na mabenki ya biashara ambayo yako chungu nzima nchini. Bunge hili pia hadi hii leo limeshindwa kufuatilia wizi uliofanywa na fisadi Mkapa na fisadi Yona wa kukupua Mgodi wa Kiwira ambao baada ya kufanyiwa tathmini na wataalamu ulionekana una tamani ya shilingi bilioni 7, lakini mafisadi hao waliamua kujiuzia mgodi huo kwa 10% tu ya thamani yake na ambayo ni sawa na shilingi milioni 700 kulipa 1% ya thamani ya mgodi huo ambayo ni sawa na shilingi 70 millioni. Pia bunge hilo limeshindwa kufuatilia ukwapuaji wa nyumba ulioidhinishwa na fisadi Mkapa kwa kushirikiana na mafisadi wenziye katika awamu yake wa kuuza nyumba za serikali kwa bei ya kutupa. Ukwapuaji huo umesababisha serikali kuingia hasara ya shilingi bilioni 200. Bunge hili pia hadi hii leo limeshindwa kufuatilia ahadi za Waziri Mkuu Pinda katika kutekeleza mapendekezo ya kamati ya Mwakyembe kuhusiana na ufisadi wa Richmond ambapo pia waliishauri serikali kuwaondoa Mkuu wa TAKUKURU Edward Hosea na Mwanasheria Mkuu Mwanyika Bunge hili limeshindwa kufuatilia kelele za Watanzania kuhusiana na mikataba ya uchimbaji madini yetu ambayo haina maslahi yoyote kwa Watanzania ambayo mingi ilisainiwa katika awamu ya tatu. Mikataba ya uchimbaji wa dhahabu, Tanzanite na hata almasi zetu. Pia kama mtakumbuka hivio karibuni tumeona juhudi kubwa za Sitta kuzuia mijadala mizito kuhusiana na mambo mbali mbali yenye maslahi makubwa kwa Watanzania kama ule mradi wa vitambulisho ambao inasemekana utagharimu shilingi 200 bilioni na kuchunguzwa kwa ufisadi mkubwa uliofanywa na makapuni ya Meremeta na Tangold labda na deep green ambapo at least shilingi 155 bilioni kama siyo zaidi zilikupuliwa na mafisadi. Sasa kwa visingizio ambavyo havina kichwa wala miguu Sitta na Pinda wanadai kwamba Meremeta na Tangolod inalihusisha jeshi letu na hivyo hilo linagusa 'usalama wa Taifa' hivyo wizi huo mkubwa wa shilingi 155 bilioni haustahili kujadiliwa wala kuchunguzwa na yeyote yule nchini. Kwa ushahidi niliotoa hapo juu mimi naamini kabisa Bunge letu ukiondoa wabunge wachache ambao hawafiki hata 10% ya Wabunge wote limepoteza mwelekeo na halistahili tena kuitwa "Bunge Tukufu la Tanzania" kwani utukufu huo umeshapotea miaka mingi sasa. Hili linastahili kuitwa Bunge la Mafisadi Tanzania maana siku zote liko mstari wa mbele kuficha madhambi ya mafisadi waliojaa tele katika serikali ya awamu ya tatu na hii iliyopo madarakani na pia wamejaa tele ndani ya Chama Cha ....... Hili Bunge letu sasa linastahili kuitwa Bunge Har........ la ....... mtajijua! Mungu ibariki Tanzania Tafakari!

No comments:

Post a Comment