Friday, August 24, 2012

Polisi kufunguka leo kuhusu kilichomkuta Dk Ulimboka

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, leo watazungumzia hatua ilizofikia katika uchunguzi wa tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven Ulimboka. Pamoja na suala la Dk Ulimboka, imesema pia itazungumzia mambo kadhaa yanayohusu usalama wa nchi. Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliliambia gazeti hili kuwa atazungumzia suala la Dk Ulimboka ili kuweka wazi kwa umma kuhusu tukio hilo lililokuwa gumzo katika siku za hivi karibuni. Kamanda Kova alitoa kauli hiyo alipotakiwa na gazeti hili kueleza endapo Dk Ulimboka ni mmoja wa mashahidi katika kesi iliyokwishafunguliwa kuhusu tukio la kutekwa kwake. “Tutazungumza na wananchi na wanahabari kwa ujumla kuhusu mambo mengine yanayohusu usalama wa nchi pamoja na hatua tulizofikia katika uchunguzi wa kitendo cha kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka,” alisema Kova. Hata hivyo, Kova hakutaka kuzungumzia suala la mtu anayedaiwa kujitokeza na kukiri kuwa ndiye mtekaji wa Dk Ulimboka na yale yaliyoandikwa katika gazeti la Mwanahalisi akidai kuwa mambo hayo yapo mahakamani. “Sisi tutaweka wazi wajibu tulioufanya na hatua tulizofikia kuhusu kutekwa kwake, mambo mengine ni ya kimahakama, hatuwezi kuyaingilia,” alisema Kova. Kova aliwataka Watanzania kuliamini Jeshi la Polisi na kusisitiza kuwa linafanya kazi yake kwa uadilifu na litahakikisha kuwa ukweli kuhusu tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi, unafahamika.  

Kutekwa kwa Dk Ulimboka 
Dk Ulimboka ambaye anatajwa kuwa kinara wa mgomo wa madaktari, alitekwa usiku wa Julai 26 mwaka huu na kujeruhiwa vibaya, kisha kutelekezwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Kutokana na tukio hilo, daktari huyo wa magonjwa ya binadamu alitibiwa kwa muda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Tangu arejee nchini, Dk Ulimboka amekuwa kimya na mara kadhaa akigoma kuzungumzia yaliyomtokea akisisitiza kuwa muda wa kufanya hivyo haujafika. Lakini wakati daktari huyo akigoma kueleza kilichomsibu, wanaharakati wa masuala ya binadamu wameshatoa tamko kuituhumu Serikali kwamba inahusika, na hivyo kuitaka ilifungulie gazeti la Mwanahalisi walilodai kuwa lilifungwa kutokana na kuandika ukweli kuhusu tukio hilo.

No comments:

Post a Comment