Friday, August 24, 2012

WACHEZAJI WAVUTA BANGI KUKIONA-TFF

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema litaanza kufanyia kazi kwa vitendo tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya hususan bangi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wachezaji hapa nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili ni kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya wachezaji wanatumia bangi, ingawa bado hawajapata ushahidi.
“Tunasikia, lakini hatuna ushahidi, kwamba vijana wetu wanatafuna bangi, ila viongozi wengi wamekuwa wakilisemea pembeni, sisi kama wazazi jukumu letu ni kuwaelimisha juu ya athari zake, maana wao wanaotumia wanaweza kuona inawaongezea hamasa, lakini hawajui madhara yake,” alisema Tenga.
Alisema wameagiza suala hilo lianze kufanyiwa kazi katika timu ya taifa, Taifa Stars na Ligi Kuu Bara, ambako viongozi wanapaswa kukaa chini na vijana wao kuwapa elimu nasaha, kabla ya kuanza kuchukuliwa hatua.
“Bangi na mpira ni vitu viwili tofauti, tumeagiza elimu ianze kutolewa kuanzia national team (timu ya taifa) na Premier League (Ligi Kuu), ikiwezekana waletewe hata wataalamu waweze kuwapa elimu kabla hatujaanza kuchukua hatua, ambapo kutakuwa na testing (vipimo) ya kushtukiza na atakayekataa, kanuni zinachukua mkondo wake mara moja,” alisisitiza Tenga.
Tenga aliongeza kuwa, suala hilo litawekwa katika kanuni za Ligi Kuu na tayari Kamati ya Tiba imepewa maelekezo kuhusiana na hilo, ambapo litaanza kufanyiwa kazi mara tu elimu itakapokuwa imetolewa kwa walengwa.
Jumamosi iliyopita, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenera Mukangara pia aliwataka wachezaji chipukizi kutojiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya wakati akitoa zawadi kwa washindi wa michuano ya BancABC SUP8R, ambapo Simba walitwaa ubingwa.
Katika hatua nyingine, Tenga ameelezea kufurahishwa na hamasa iliyoko katika usajili hapa nchini, lakini akakosoa watu wasio wataalamu wa ufundi kuendesha zoezi hilo, badala ya makocha au kamati za ufundi.
Alisema walikubaliana kuruhusu usajili wa nyota kutoka nje kwa lengo la kuhamasisha ushindani hapa nchini, kwani njia nzuri ya kumpa ujuzi mchezaji ni kumpa nafasi kucheza na yule aliye mzuri zaidi.
“Utamaduni duniani kote, usajili unafanywa na kocha, lakini hapa mchezaji anasajiliwa na mdhamini au kiongozi, mambo ambayo hujiingiza kwenye matatizo, timu ikifungwa wanachama wanakufuata nyumbani. Mi huwa nashangaa timu ikifungwa watu wanavamia viongozi, kumbe hatujajiweka vizuri,” alisema.
Tenga alitaka wataalamu ndio wapewe jukumu hilo, huku akisisitiza kuwa, vijana wenye vipaji ambao wapo hivi sasa hapa nchini wapewe nafasi na si lazima kukimbilia nje, labda iwe kwa mchezaji mzuri zaidi.
Chanzo: Tanzania Daim

No comments:

Post a Comment